Tuwakumbuke
Mashujaa wa nchi yetu
Wazalendo halisi wa Kenya
Jinsi walivyokuwa wamejitolea mhanga
Kupambania uhuru na ukombozi wa nchi yetu:
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu ya kila aina
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Tuwakumbuke mashujaa wa Pwani ya nchi yetu
Wazalendo wa Mombasa na Malindi na Lamu
Na Siu na Pate na Vanga....
Ambao mamia ya miaka iliyopita
Walikufa wakipambana
Wakipambana dhidi ya uvamizi wa Waarabu
Waliokataa kutawalwa na wageni
Walioupiga vita uvamizi wa kikatili wa Wareno
Wareno wakashindwa kabisa kupenya hadi bara
Tukumbuke kuwa ngome
Inayoitwa Fort Jesus
Ambayo sasa ni jumba la ukumbusho Mombasa
Ngome ni taswaira ya uvamizi wa Wareno nchini
Ni ushahidi wa upinzani kutoka kwa mababu na mabibi zetu
Ni ukumbusho wa nyanyaso na gandamizo
Za Wazungu wa kwanza kujaribu kutawala Kenya
Ngomeni maelfu ya Wamijikenda na Waswahili walifungwa
Ngomeni wazalendo wa nchi yetu waliteswa
Ngomeni damu ya mashujaa ilimwagika
Tumtaje Shee Mvita, mfalme wa mwisho wa Mombasa
Alieuawa na Wareno
Akiutetea uhuru na ukombozi wa watu wake
Mfano wa bei ghali iliyolipwa na wazalendo
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Mwangeka
Wawa Mwangeka wa Mwanda Njawuli
Mzalendo kutoka Vuria,
Kilele cha milima ya Dawida
Milima ya juu zaidi Mashariki mwa Kenya
Inayosifika kwa uzuri wake usiyo na kifani
Ing'oni Mwangeka mzaliwa sehemu hii ya nchi yetu
Nae anatajika, ni mtu mashuhuri
Kwa uzalendo na ushujaa
Kwa kuongoza maaskari hodari wa Dawida
Waliowaeleza wakoloni kwa nyuta na mishale
Nyinyi ni nani mnaotamba katika nchi yetu?
Hii ni ardhi yetu kutoka kale na zamani
Tutaitetea hata kwa damu kumwagika
Tunapinga kutawalwa na wageni
Tuko kwa nchi yetu tunawezaje kuwafanyia kazi?
Tunaishi kwa jasho letu wenyewe
Basi itakuwaje tuwe wapagazi wezu?
Tu watu kama nyinyi tutakubalije kuwa watumwa wenu?
Tuna lugha, dini, mila na tamaduni zetu hatuna haja na zenu!
Kina Mwangeka wakatangaza vita dhidi ya vita vya wakoloni
Wakapigana wakapigana wakapigana bila kurudi nyuma
Mwangeka na maing'oni wa Dawida
Wakakataa kufa wakipiga magoti
Wakadinda kuwainulia maadui mikono yao
Wakafa wakiwa na silaha mikononi
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Halafu kuna Me Kitilili
Me Kitilili Me Kitilili Me Kitiliii
Me Kitilili wa Menza
Me Kitlili mwanamke shujaa kutoka Ugiriamani
Mzalendo Me Kitilili na Wanje, Wanje wa Mwadorikola
Jazanda ya uzalendo wa wanawake wa nchi yetu
Waliowaongoza wanaume na wanawake wa Ugiriamani
Kuuasi na kuulani ukoloni kwa maneno na vitendo
Kukataa kuwa maaskari wa wakoloni
Kugoma kufanywa mahamali wa mabeberu
Kudinda kunyang'anywa ardhi yao
Wakoloni wakawashambulia kikatili kikoloni
Wanje wa Mwadorikola na Mee Kitilili
Wakawaongoza wanaume kwa wanawake
Kutetea mila na tamaduni za Wagiriama
Kulinda hadhi ya mtu mweusi, heshima ya Mwafrika
Wakoloni wakawaita wanawake mashujaa wetu wachawi
Wakakashifiwa wakakamatwa wakadunishwa wakateswa
Mama zetu wakahamishwa hadi nchi ya Wakisii
Bali Me Kitilili na Wanje wa Mwadorikola
Wakasimama madhubuti wasitingishike wasikate tamaa
Wakatoroka na kujasiri mamia ya kilometa
Wasiogope hatari za nyika na misitu na wanyama tilatila
Wakarudi Ugiriamani kuendelea na mapambano
Wakaendelea kuongoza harakati dhidi ya ukoloni
Wakatukanwa wakapakwa matope wakazuiwa wakafungwa
Wakahamishwa hadi Kisimayu
Bali mama zetu milima ya ushujaa na uzalendo
Mfano wa ukakamavu na kujitolea mhanga
Wakakataa kusalimu amri za wakoloni
Wakatetea uhuru wa nchi yetu na watoto wao daima
Wakaishi wakiwa mihimili ya umoja wa watu wao
Wakawa sehemu ya nguzo ya historia ya ukombozi wa Kenya
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Huko Unandini Koitaleli ni mashuhuri
Koitaleli, kiboko cha kiburi cha wakoloni
Wanandi kwa mikuki na ngao mikononi
Wakawauliza wakoloni:
Hii ni nchi yetu kutoka tangu na tangu
Nani amewaruhusu kujenga reli hapa?
Mnawezaje kuingia na kupita kwetu
Bila hata hodi wala hamjambo!?
Mna njama gani juu ya ardhi yetu
Ambapo tumekuwa tukiishi tangu kale na zamani!?
Wakoloni kwa kiburi kujitapa na kujisahau
Wakajibu kwa bunduki na bomubomu
Kwa kuua na kuchinja pasina kutangaza vita
Wanandi wakatahamaki wakajizatiti sawasawa
Wakasema hawa watu ni wa sampuli gani?
Watu gani hawa wasio na heshima wala adabu!
Ni binadamu gani hawa wasiojali maisha?
Hawajui lugha nyingine ila vita na madharau tu!
Basi, imetupasa kupigana nao
Kwani nasi hatuna utamaduni wa woga
Ndipo Wanandi wakajiandaa ipasavyo
Kwa mikuki na ngao wakajumuika
Mabingwa wa vita vya kigorila wakajipanga barabara
Wakawa wanawavizia na kuwashambulia ghaflaghafla wachokozi
Kina Koitaleli wakawachapa wavamizi hadi wakasarenda
Wakatapika kiburi chao wakaomba majadiliano
Mwafrika, mtu mweusi, akawafanya wainue mikono
Ikawa hawana budi ila kuitisha majadiliano ya amani
Ela Koitaleli alipoenda kujadiliana na mabeberu akauawa
Shujaa Koitaleli akauawa kwa mizungu ya Wazungu ya kioga
Bali kina Semoi wakachukua nafasi yake
Mapambano dhidi ya ukoloni yakaendelea
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Tunajivunia Waiyaki
Waiyaki Waiyaki Waiyaki
Waiyaki wa Dagoreti
Chimbuko cha mapambano ya Wakikuyu dhidi ya walowezi
Damu iliyozaa Jeshi la Uhuru na Mashamba, Mau Mau
Kina Waiyaki walipinga unyonyaji wa makampuni ya kibeberu
Walisema hapana kwa ubepari nchini
Hapana kwa mfumo wa kiuchumi wa unyonyaji wa mtu kwa mtu
Walivamia ngome za kupanda mizizi ya mirija ya ubeberu Kenya
Wazalendo wa nchi yetu waliasi kupunjwa na wageni
Wakakataa na utu wa Mwafrika kwa silaha
Waiyaki akakamatwa kuhamishwa Pwani
Wakamshawishi wakamtisha wakamtesa ili asarende
Wapi! wakapiga ukuta kwa babu yetu
Wakashindwa kuumwaga uzalendo wa Mkenya halisi
Wasiweze hata kuukwaruza uhodari wake
Ufashisti wa wakoloni ukazidi kudhihirika Kibwezi
Walipomzika shujaa wetu Waiyaki akiwa hai
Miungu ya nchi yetu
Waingereza walimzika mzalendo akiwa bado anaishi!
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Nyanjiru
Oh Nyanjiru
Tumkumbuke Mary Muthoni Nyanjiru
Yule mwanamke jasiri wa enzi za kiburi cha walowezi
Nyakati za ushujaa wa Harry Thuku
Siku za kukataa kubeba vipande vya wakoloni
Kudinda kulazimishwa kuwafanyia kazi masetla
Kugomea mishahara duni ya kitumwa
Kupinga kunyonywa na kunyanyaswa kwa wanawake
Enzi za chimbuko cha vyama vya kupigania uhuru
Hizo enzi za East African Association
Mapambano ya wafanyikazi katika miji ya nchi yetu
Mapambano dhidi ya kina Colonel Grogan na Lord Delamare
Wakati unyama wa wakoloni dhidi ya wananchi
Ulikuwa ni sehemu ya maisha ya kila siku
Tukitukanwa na kufungwa na kuteswa kiholela
Tukitemewa mate na Wazungu vururumtende
Tukidhihakiwa na kudhalilishwa
Na kina memsahibu walokuwakitamba mijini na mashambani
Sisi watu weusi tukifanywa watu wa mwisho
Kana kwamba Kenya si nchi yetu wenyewe
Hizo nyakati za kupinga kulipa kodi kwa wavamizi
Harry Thuku akakamatwa na kuwekwa ndani
Wanaume na wanawake wa Nairobi wakaandamana
Harry Thuku na wafungwa wote wa kisiasa wawachiliwe!
Wafunguliwe mara moja tena bila masharti!
Nje ya Norfolk Hotel
Karibu na Chuo Kikuu cha Nairobi
Si mbali na Central Police Station
Siku hiyo mwaka wa 1922
Kina Nyanjiru walikata shauri kuandamana hapo
Hadi shujaa wao atakapofunguliwa
Wakalala hapo kwa siku na masiku
Baridi ya usiku wakivumilia na njaa na kiu pia
Vitisho vya walowezi wasikubali viwatishe
Bezo za kishenzi za kuuzi za wavamizi wakazipuuza
Na hata wanaume walipozubaa na kusitasita
Walipolegalega na kushindwa kutoa uongozi thabiti
Mary Muthoni Nyanjiru hakulimatia, alijitokeza kimoja
Akadai wanaume wavue surwale na kuvaa skati
Wawape wanawake surwale zao wazivae
Ndipo wanawake wakawa katika msitari wa mbele
Wanaume wakifuata nyuma katika harakati za ukombozi
Pamoja wakasonga mbele kumfungulia mpendwa wao
Pamoja wakaandika historia ya uhuru wetu-kwa damu yao
Shujaa Mary Muthoni Nyanjiru
Akawa wa kwanza kuangushwa na risasi za polisi wa kikoloni
Makaburu waliokuwa wakistarehe Norfolk Hotel
Huku wakiwatukana na kuwakebehi watu wetu
Wakachukua silaha zao kwa furaha za wehu
Wakaungana na polisi wao kufanya mito ya damu Nairobi
Kutoka kwa mamia ya dada na kaka zetu
Bali yote hayo hayakuzima moto wa mapambano ya uhuru
Ukaendelea kuwaka moto wa uhuru ukazidi kuzagaa
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Tumkumbuke Makhan Singh
Komredi Makhan Singh, mkomunisti wa kwanza Kenya
Sehemu ya harakati za wafanyikazi dhidi ya ukoloni
Sogora wa mbinu na hila za kuzatiti mapambano
Mapambano ya wavujajasho dhidi ya mabepari
Katika historia ya vyama vya kimaendeleo vya wafanyikazi
Jina la mwanamapinduzi Makhan Singh litang'aa daima
Makhan Singh, sehemu ya kina Chege Kibacia
Chege Kibacia na mashujaa wa watiririkajasho
Makhan Singh,alieaminika hata KAU ya Kiburi House
KAU ya Mau Mau katika Kiburi House
Ndiyo, tusisahau Kiburi House
Kiburi House, walikokuwa wakikutana kina Bildad Kaggia
Kina Eliud Mutonyi na kina Isaac Gathanju
Kiburi House, kulikokuwa kukipangwa njama za Mau Mau
Ngome ya waliochagua barabara ya mapinduzi
Walimtambua Makhan Singh Kiburi House walimhesabu
Kina Makhan Singh na Pio Gama Pinto na Alibhai Mulla Jeevanjee
Wazalendo wa Kenya wa asili ya Kihindi
Waliowaambia Wahindi wa Kenya
Enyi wananchi wenzetu wa asili ya India
Tahadharini msiwe mapopo na vinyonga
Epukaneni na kuwa makupe na makunguni wa nchi hii
Ikiwa Kenya ni nchi yenu
Kama mnajihesabu raia wa nchi hii
Unganeni na Wafrika kupigania uhuru wa Kenya
Kuweni sehemu ya wazalendo wanaodai ukombozi
Msikubali kutumiwa kunyonya na kufukarisha taifa hili
Kataaeni kuwa upande wa wakoloni na wadhalimu
Msijidanganye kuwa nyinyi ni bora kuliko wenyeji
Wafanyikazi wote tunanyonywa haya shime tuungane
Tuwe na mshikamano dhidi ya wanyonyaji
Tusikubali ubaguzi wa rangi utuvunjie umoja wetu
Tuugomee ukabila usitumiwe kuondoa uwezo wetu
Wala tusikubali migawanyiko ya kijinsia iturudishe nyuma
Kenya na Uganda na Tanzania wafanyikazi tuwe kitu kimoja
Wafanyikazi wote tupambanie taifa la Afrika Mashariki
Afrika Mashariki ya kimapinduzi
Afrika Mashariki inayopinga ukoloni-mamboleo
Afrika Mashariki ya mfumo kwa kisoshalist
Afrika Mashariki itakuwa nguvu kubwa za kisiasa na kiuchumi
Afrika Mashariki itakuwa matumaini ya uhuru na ukombozi kamili
Sauti ya Makhan Singh, sauti ya wanaonyanyaswa
Iliyoitikiwa na wafanyikazi na umma wa wazalendo
Iliwafanya wakoloni kujikojolea na kujiharia
Makhan aliwakosesha mabepari wa Afrika Mashariki usingizi
Jina lake likaandikwa katika kitabu cheusi cha dola la kikoloni
Na hali ya hatari ilipotangazwa rasmi
Makhan Singh hakusahauliwa na kifagio cha polisi wa kikoloni
Makhan Singh alikamatwa mara moja
Makhan Singh akafungiwa kizuizini
Makhan Singh alifungwa miaka kumi kizuizini
Kwa sababu ya harakati za wavujajasho alifungwa Makhan Singh
Alifungwa kwa ajili ya uhuru wa taifa letu
Bali bendera ya wakoloni iliposhushwa Kenya
Na bendera ya Wakenya kupandishwa
Kupandishwa na mapambano ya kina Makhan Singh
Serikali ya msaliti Jomo Kenyatta na mahomugadi
Ilimchukuwa Makhan kana kwamba si lolote si chochote nchini
Bali kutambuliwa na wanyapara wa mitaji ya mabeberu Kenya
Kupigana pambaja na wanyonyaji na wagandamizaji wa wafanyikazi
Haikuwa nia ya komredi Makhan Singh, mwanamapinduzi
Makhan Singh alikufa akiandika historia ya mapambano
Historia ya mapambano ya wafanyikazi wa Kenya
Makhan Singh ....Makhan Singh....Makhan Singh.......
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Mau Mau
Mau Mau, jeshi la Uhuru na Mashamba
Kilele cha mapambano dhidi ya ukoloni-mkongwe
Jazanda ya wazalendo na uzalendo
Mau Mau, mashujaa halisi wa nchi yetu
Wakakataa kutembea katika njia ya kina Jomo Kenyatta
Njia ya wasabili ya kuomba uhuru wa kuomba
Njia ya kutegemea adili ya wagandamizaji
Njia ya kuongozwa na masilahi ya ulafi na uroho
Njia ya kukana mapambano ya silaha katika hali ya ufashisti
Mau Mau wakulima na wafanyikazi wa Kenya
Wanaume kwa wanawake wazee kwa vijana
Walichagua barabara ya kimapinduzi ya uhuru
Mau Mau waliokula kiapo cha ukombozi
Kiapo cha kuwaunganisha na kuwashikanisha kwa mapambano
Mapambano ya kupigania mashamba na uhuru wetu
Mapambano ya kupigania heshima na utu wa mtu mweusi
Mapambano ya demokrasi na haki za binadamu
Mapambano ya kuung'oa ukoloni nchini kwetu
Maelfu kwa maelfu ya wazalendo wa Kenya
Waliowacha kila kitu na kuitikia mwito
Mwito wa kujitoma milima Kenya na Nyandarua
Mwito wa kusambaa katika miji na vijiji vya nchi yetu
Kuendeleza vita vya kigorila dhidi ya wakoloni na vibaraka vyao
Waliovumilia njaa na kiu na baridi na upweke na dhiki tilatila
Wakajasiri kuwindwa na kukamatwa na kuhamishwa
Waliokuwa tayari kuvumilia kukamatwa na kufungwa
Mau Mau, maelfu kwa maelfu waliwawa na wakoloni
Mau Mau, ni wangapi mashujaa wetu waliyonyongwa!
Mau Mau, kiboko cha makaburu na mahomugadi
Mau Mau, kwa damu yenu, kwa kujitolea mhanga kwenu
Enyi wananchi wakereketwa wa taifa letu
Kwa msimamo wenu
Kwa mwelekeo wenu
Kwa harakati zenu
Kwa vita sahihi mlivyopigana
Tuko pahali tulipo sasa, hatua kubwa mbele
Ukoloni-mkongwe haupo tena nasi, mliukwamua Mau Mau
Kwenu Afrika ikapata mfano mzuri wa kuiga
Mfano wa kupigania ukombozi kwa kutumia silaha
Mau Mau, Jeshi la uhuru na Mashamba
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu ya kila aina
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Mau Mau
Vilikuwa vita vya kupigania uhuru wa kitaifa
Vita vya wananchi na wananchi kwa ajili ya wananchi
Navyo vita vya wananchi vilizaa mashujaa wengi, wengi sana
Mashujaa waliochipuka katika msitari wa mbele
Mashujaa walioteuliwa na ari na shauku ya kujitolea mhanga
Kujitolea mhanga kutumikia vita vya ukombozi
Mashujaa waliodhihirisha ujemedari na uhodari
Wa kuongoza jeshi lililokuwa la wananchi wa Kenya
Mashujaa waliokuwa mashuhuri katika uwanja wa vita
Kwa usanii wa kuzalisha hila na mbinu za kuwachapa maadui
Mashujaa wa siasa na itikadi ya wanaonyanyaswa
Waliohamasisha umma kwa maneneo na vitendo vyao
Mashujaa wa kutetea haki na ukweli na maslahi ya wengi
Waliochagua kuishi maisha ya utu ya kupinga dhuluma
Mashujaa kwa mapenzi ya nchi yetu na ukombozi wake
Kwa maendeleo ya Kenya na furaha ya kila raia
Kwa imani na amani ya wanaonyonywa na kunyanyaswa
Mashujaa waliokuwa wakipiga konde nyoyo kila wakati
Waliopambana dhidi ya kulegalega na kukata tamaa
Mashujaa ambao baada ya kukamatwa na wakoloni
Wakiwa mikononi mwa makaburu na mahomugadi
Wakiteswa katika magereza ya wadhalimu wa nchi yetu
Katikati ya ufashisti wa dola la Waingereza
Walivumilia yote kwa ujasiri usiyo na kifani
Walikataa kusaliti kiapo cha kupigania uhuru
Wakadinda kukana vita vya haki vya ukombozi wa Kenya
Wasikubali kutoboa siri wala kusaliti makomredi wao
Na hata waliponyongwa na kuuawa kinyama kabisa
Mashujaa wetu walikufa kwa fahari
Wakawawachia wakoloni na vibaraka wao aibu ya milele
Ni wengi mashujaa wa Mau Mau, wengi sana
Kwani Mau Mau ni wanati, wananchi wazalendo wakereketwa
Mau Mau, ushujaa wa mamilioni
Ya wakulima na wafanyikazi
Wanaume kwa wanawake wazee kwa vijana
Ambao kwa moyo wa harambee uzalendo na kujitegemea
Walifunga sura ya ukoloni-mkongwe katika nchi yetu
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu ya kila aina
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona