Mau Mau
Mau Mau, jeshi la Uhuru na Mashamba
Kilele cha mapambano dhidi ya ukoloni-mkongwe
Jazanda ya wazalendo na uzalendo
Mau Mau, mashujaa halisi wa nchi yetu
Wakakataa kutembea katika njia ya kina Jomo Kenyatta
Njia ya wasabili ya kuomba uhuru wa kuomba
Njia ya kutegemea adili ya wagandamizaji
Njia ya kuongozwa na masilahi ya ulafi na uroho
Njia ya kukana mapambano ya silaha katika hali ya ufashisti
Mau Mau wakulima na wafanyikazi wa Kenya
Wanaume kwa wanawake wazee kwa vijana
Walichagua barabara ya kimapinduzi ya uhuru
Mau Mau waliokula kiapo cha ukombozi
Kiapo cha kuwaunganisha na kuwashikanisha kwa mapambano
Mapambano ya kupigania mashamba na uhuru wetu
Mapambano ya kupigania heshima na utu wa mtu mweusi
Mapambano ya demokrasi na haki za binadamu
Mapambano ya kuung'oa ukoloni nchini kwetu
Maelfu kwa maelfu ya wazalendo wa Kenya
Waliowacha kila kitu na kuitikia mwito
Mwito wa kujitoma milima Kenya na Nyandarua
Mwito wa kusambaa katika miji na vijiji vya nchi yetu
Kuendeleza vita vya kigorila dhidi ya wakoloni na vibaraka vyao
Waliovumilia njaa na kiu na baridi na upweke na dhiki tilatila
Wakajasiri kuwindwa na kukamatwa na kuhamishwa
Waliokuwa tayari kuvumilia kukamatwa na kufungwa
Mau Mau, maelfu kwa maelfu waliwawa na wakoloni
Mau Mau, ni wangapi mashujaa wetu waliyonyongwa!
Mau Mau, kiboko cha makaburu na mahomugadi
Mau Mau, kwa damu yenu, kwa kujitolea mhanga kwenu
Enyi wananchi wakereketwa wa taifa letu
Kwa msimamo wenu
Kwa mwelekeo wenu
Kwa harakati zenu
Kwa vita sahihi mlivyopigana
Tuko pahali tulipo sasa, hatua kubwa mbele
Ukoloni-mkongwe haupo tena nasi, mliukwamua Mau Mau
Kwenu Afrika ikapata mfano mzuri wa kuiga
Mfano wa kupigania ukombozi kwa kutumia silaha
Mau Mau, Jeshi la uhuru na Mashamba
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu ya kila aina
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Mau Mau
Vilikuwa vita vya kupigania uhuru wa kitaifa
Vita vya wananchi na wananchi kwa ajili ya wananchi
Navyo vita vya wananchi vilizaa mashujaa wengi, wengi sana
Mashujaa waliochipuka katika msitari wa mbele
Mashujaa walioteuliwa na ari na shauku ya kujitolea mhanga
Kujitolea mhanga kutumikia vita vya ukombozi
Mashujaa waliodhihirisha ujemedari na uhodari
Wa kuongoza jeshi lililokuwa la wananchi wa Kenya
Mashujaa waliokuwa mashuhuri katika uwanja wa vita
Kwa usanii wa kuzalisha hila na mbinu za kuwachapa maadui
Mashujaa wa siasa na itikadi ya wanaonyanyaswa
Waliohamasisha umma kwa maneneo na vitendo vyao
Mashujaa wa kutetea haki na ukweli na maslahi ya wengi
Waliochagua kuishi maisha ya utu ya kupinga dhuluma
Mashujaa kwa mapenzi ya nchi yetu na ukombozi wake
Kwa maendeleo ya Kenya na furaha ya kila raia
Kwa imani na amani ya wanaonyonywa na kunyanyaswa
Mashujaa waliokuwa wakipiga konde nyoyo kila wakati
Waliopambana dhidi ya kulegalega na kukata tamaa
Mashujaa ambao baada ya kukamatwa na wakoloni
Wakiwa mikononi mwa makaburu na mahomugadi
Wakiteswa katika magereza ya wadhalimu wa nchi yetu
Katikati ya ufashisti wa dola la Waingereza
Walivumilia yote kwa ujasiri usiyo na kifani
Walikataa kusaliti kiapo cha kupigania uhuru
Wakadinda kukana vita vya haki vya ukombozi wa Kenya
Wasikubali kutoboa siri wala kusaliti makomredi wao
Na hata waliponyongwa na kuuawa kinyama kabisa
Mashujaa wetu walikufa kwa fahari
Wakawawachia wakoloni na vibaraka wao aibu ya milele
Ni wengi mashujaa wa Mau Mau, wengi sana
Kwani Mau Mau ni wanati, wananchi wazalendo wakereketwa
Mau Mau, ushujaa wa mamilioni
Ya wakulima na wafanyikazi
Wanaume kwa wanawake wazee kwa vijana
Ambao kwa moyo wa harambee uzalendo na kujitegemea
Walifunga sura ya ukoloni-mkongwe katika nchi yetu
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu ya kila aina
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Kimaathi
Dedan Kimaathi
Dedan Kimaathi wa Waciuri
Mkuu wa jeshi la Uhuru na Mashamba
Kati ya majemedari wa Mau Mau Kimaathi ali ni gogo
Baina ya mashujaa wa uhuru hakika Dedan Kimaathi ni nyota
Nyota iliyoonekana na inayoonekana katika kila pembe ya Kenya
Nyota inayong'aang'aa Afrika kuonyesha barabara sahihi
Barabara ya kimapinduzi ya kuelekea kwa uhuru
Nyota mashuhuri Afrika na hata duniani kote
Kwa wanaonyonywa na kugandamizwa
Oh pande la mwana wa Kenya, ndugu yetu mpendwa Kimaathi
Ni maneno gani tutayatumia ewe mwana wa Waciuri
Hata tukaeleza sifa zako tilatila kwa kikamilifu?
Ninashindwa hata kupata nahau bora
Za kuandika kuhusu Mkuu wa Jeshi la Uhuru na Mashamba
Pengine niseme tu kuwa Kimaathi alikuwa mtu
Alikuwa mtu Kimaathi, mtu kama sisi
Alikuwa na mamaye na babaye na bibiye na babuye
Alikuwa na jamaaze, damuye, kama sisi
Alikuwa na mke, mke aliempenda sana, tena sana
Kimaathi alikuwa kijana, kijana kama sisi
Kijana alietambua jukumu lake kama mwananchi mzalendo
Mtu ambae alifahamu yu mtu kwa maneno na matendo
Kimaathi, maana ya mapenzi kwa nchi yako na watu wake
Kimaathi, mfano halisi wa ushujaa wa kimapinduzi
Ushujaa wa umma uhodari wa maslahi ya wanaogandamizwa
Kimaathi, twasira na jazanda ya kujitolea mhanga
Kwa uhuru na ukombozi wa kitaifa
Kati ya wasanii wa hila na mbinu ya vita vya kigorila
Kimaathi wa Waciuri anatajika kama msanii mkubwa
Kati ya majina yaliyokuwa yakiogopewa na wakoloni
Jina la Dedan Kimaathi lilikuwa namba wani
Kimaathi aliwafanya makaburu kujikojolea na kujiharia
Wanyonyaji wakashindwa kula manyonyaji yao kwa amani
Wangapi walowezi walifungasha na kuondoka
Kwa kuogopa Kimaathi, asakari hodari wa Mau Mau!
.....ahhhh! lakini nani asiemfahamu Kimaathi nchini!
Ni mwananchi gani mzalendo ambae hajui Mau Mau!
Ni historia gani ya Kenya hiyo ambayo haitaji Mau Mau!
Ni mashujaa gani wa Kenya unawajua kama humjui Kimaathi!
Hakika katika kuandika historia sahihi ya taifa letu
Hatutawasamehe kina Ndirangu Mau milele
Kina Ndirangu Mau- mahomugadi waliyomsaliti shujaa wetu
Kina Ndirangu Mau- kina Kenyatta na Moi wenye dola la kisaliti
Kina Ndirangu Mau- wanyonyaji wa wakulima na wafanyikazi
Kina Ndirangu Mau- vibaraka wa mabeberu
Kina Ndirangu Mau- wanaopinga ukombozi wa taifa letu
Tutawasemehe vipi kwa kuendelea kukataa kumzika Kimaathi!?
Mnamo tarehe 18 Februari, 1957
Katika Jela ya Nairobi
Dedan Kimathi wa Waciuri, shujaa mkuu wa Kenya
Alinyongwa na wakoloni wa Waingereza
Alinyongwa baada ya mateso ya kifashisti ya kina Ian Henderson
Alinyongwa huku akipambana akiwa na pingu mikononi
Shujaa wa nchi yetu alikufa akipigana
Mwili wa Kimaathi ulitupwa na wakoloni
Katika Jela ya Kamiti
Na hadi wa leo
Mazishi ya Mzalendo Kimathi
Yanangojea kufanywa, tukumbuke
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu ya kila aina
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Mwamdawiro Mghanga, Mwenyekiti wa CPK
Jela Kuu ya Kibos 04-06-198







