“Utekelezaji wa sera za kibepari nchini umetuumiza sisi wananchi tuliyo wengi. Ubinafsishaji wa ardhi, migodi, mbuga za wanyamapori na maliasili zingine umetupora sisi tuliyo wengi haki za umilikaji na matumizi ya ardhi zetu za jadi tulizozirithi kutoka kwa mabibi na mababu zetu. Badala yake serikali inashirikiana na wawekezaji (mabepari) wa nchini na wa kigeni kutunyonya, kutunyanyasa, kutuvunjia heshima, kuvuraga utamaduni wetu na haki zetu za binadamu kiholela. Mfumo wa ubepari na ubinafsishaji unaoendelea hauwezi kutukomboa kutoka kwa ufukara na kutuletea maendeleo endelevu kwani unapanua pengo kati ya matajiri na masikini. Lazima tujizatiti na kuungana kupambania kurudi kwa Azimio la Arusha!”.
Hayo na mengine yalisemwa na kuazimiwa na jamii za wakulima, wachungaji, mashirika ya umma na Watanzania makabwela ambao walishiriki katika Kongamano la Saba la tamasha ya wasomi ya kumuenzi baba wa taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kongamano hilo lililofanyika kutoka tarehe 13 hadi 15 Aprili mwaka huu katika Ukumbi wa Nkuruma katika Chuo Kikuu cha Dar - es - saalamu liliandaliwa na Kigoda cha Nyerere chuoni hicho chini ya uwenyekiti wa Profesa Peminah Mlama. Pamoja na watu kutoka mashinani, Kongamano hilo lilishirikisha wasomi na wanafunzi wa chuo kikuu na wa shule za upili ambao walilalamika jinsi wawoto wa makabwela wanavyozidi kunyimwa fursa ya kupata elimu bora kutokana na ubinafsishwaji wa taasisi za elimu nchini Tanzania. Wanafunzi wa chuo kikuu walilalamika kuhusu ukame wa demokrasi ya kitaaluma katika vyuo vikuu iliyoandamana na ubinafsishwaji wa elimu katika nchi hiyo. Kongamano hilo lilisisimuliwa na wanafunzi wa shule za upili waliyolalamika kwa ufasaha kuwa elimu sasa inawafundisha watoto maadili ya ubinafsi, ulafi na kutojali binadamu wengine badala ya yale ya kiutu na kizalendo yaliyokuwa yakifundishwa na mwasisi wa taifa lao, Nyerere.
Wawakilishi wa jumuia za wakulima na wachungaji kutoka Loliondo, Kilosa, Mbeya, Geita walieleza kwa uchungu kuhusu masaibu wanayolazimika kuishi nayo kutokana na kunyanyaswa na kuporwa haki juu ya ardhi na maliasili zao na wawekezaji wa Kitanzania na kigeni ambao sasa wanapendelewa na serikali dhidi ya jumuia. Kongamano lilisikitishwa na maelezo kuhusu uvunjwaji wa haki za binadamu za wakulima na wachungaji wanaoishi katika maeneo ya migodi ya Geita, Shinyanga na Mwanza. Kilio hichihicho kililiwa na wakulima makabwela wa mpunga kutoka Mbeya waliyonyang’anywa ardhi zao na wajasiriamali na serikali. Pia jumuia za wakulima na wachungaji za Kilosa katika Mkoa wa Morogoro zilisimulia jinsi dhuluma na migogoro ilivyozidi sehemu zao kutokana na uvamizi na unyakuzi wa ardhi unaoendelea kutokana na ubinafsishaji.
Aidha, wanaharakati wa kupigania haki za kijamii kutoka Kampala na Moroto Uganda walishiriki na vilevile mashirika ya umma ya Kenya mkiwemo shirika la haki za kijinsia, shirika la kupigania haki ya maji na shirika la kupigania haki ya ardhi ya umma huko Garissa. Nikiwa mwenyekiti wa chama cha Social Democratic Party of Kenya (SDP) niliongoza ujumbe wa wanachama wanne kushiriki kongamano hilo maarufu.
Mada kuu ya kongamano hilo ilikuwa ubinafsishaji na haki za kijamii. Shabaha ya mada hii ilikuwa ni kutathmini athari za kiuchumi, kisiasa, kijamii na kitamaduni za marekebisho ya kiuchumi yaliyotoa Tanzania kutoka barabara ya Azimio la Arusha (ujamaa) na kuitia katika barabara ya ubeparimamboleo. Baada ya Nyerere kung’atuka kutoka kwa urais wa Jamhuri ya Tanzania na pia uwenyekiti wa chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM), rais Ali Hassan Mwinyi aliyechukua nafasi yake alianza marekebisho ya kiuchumi ya kibepari katika nchi hiyo. Rais Benjamini Mkapa alimrithi Mwinyi na kuendelea kuzingatia sera za Rais Mwinyi za ruksa ya kuuvunja mfumo wa ujamaa na kujitegemea na kuelekeza Tanzania katika mfumo wa ubepari. Hivi leo Tanzania ikiongozwa na Rais wa nne Jakayo Mrisho Kiketwe inaendelea kutekeleza sera za ubepari na ukolonimamboleo kwa fujo.
Huku ikiwa katika mfumo wa ubepari, uchumi wa Tanzania umekua kwa kasi sana (kwa zaidi ya asilimia saba). Barabara nyingi za lami zimejengwa mijini na mikoani. Katika kila miji ya Tanzania ikiwa ni pamoja na Dar - es - saalamu, Dodoma, Tanga, Mbeya, Arusha, Mwanza na Moshi majumba makubwa ya ghorofa yanaota kila kuchako. Aidha, mitaa ya kifahari wanakokaa matajiri yenye majumba makubwa na ya kupendeza ajabu nayo pia ni dhihirisho la kunoga kwa uchumi wa ubepari. Vilevile, masupamaketi ya kukidhia haja za tabaka la mabwanyenye na magari ya kifahari yamejaa kila sehemu mijini. Ardhi, migodi na mashirika ya umma yamezidi kubinafsishwa na kuuziwa (kupewa) mabepari wa Tanzania na nchi za kigeni. Wawekezaji kutoka kila pahali ulimwenguni wanakimbilia Tanzania kuwekeza na kununua mali ya umma ya viwanda, biashara, ardhi, madini, wanyamapori na maliasili zingine. Hata huduma za elimu, nyumba, maji, afya na umeme zimebinafsishwa.
Je, utekelezaji wa sera za ubepari umeathiri vipi tabaka la makabwela wa Tanzania? Washiriki wa kongamano la Nyerere walisema na kukubaliana kuwa ubinafsishaji wa uchumi kwa ujumla ni kinyume cha haki kwani unachukua mali inayomilikiwa na serikali kwa ajili ya wengi (umma) na kuwapa watu binafsi kwa kisingizio kimoja ama kingine. Marekebisho ya ubepari yamezidisha pengo kati ya matajiri na maskini, kupanda mbegu za uhasama wa kikabila na kukiuka maadili ya kiutu yaliyozingatiwa na azimio la Arusha. Rushwa imekuwa dondandugu huku unyonyaji wa mtu kwa mtu ukiwa utamaduni wa kisasa. Wakati tabaka la wachache wanaotawala wakijilimbikizia utajiri mkubwa ajabu tabaka la Watanzania wengi linazidi kudidimia katika lindi la ufukara, shida na umkosefu wa kila hali. Washiriki kutoka Kenya, Malawi, Afrika Kusini na Uganda pia walisisitiza kwamba ubinafsishaji wa uchumi katika nchi zao pia umeleta manufaa kwa tabaka la wachache tu huku tabaka la wengi likizidi kusukumwa pembeni. Mwishowe kongamano liliamua kuwa ubepari umefeli Tanzania na pia Afrika Mashariki. Watanzania wengi hawana budi kupigania kurudi kwa Azimio la Arusha la siasa ya ujamaa na kujitegemea.
Mwandawiro Mghanga, Mwenyekiti wa Social Democratic Party of Kenya (SDP), Aprili 22, 2015







